Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, likinukuu jarida La Izquierda Diario, wakosoaji wanasema Machado si tu kwamba ana historia ndefu ya kuunga mkono mapinduzi na uingiliaji wa kijeshi wa mataifa ya nje, bali pia ni mmoja wa wafuasi wa wazi wa utawala wa Kizayuni.
Uso wenye historia ya uingiliaji
Maria Corina Machado mara kadhaa amekuwa akitoa wito wa kufanyika kwa uvamizi wa kijeshi wa Marekani nchini Venezuela — kitendo ambacho hakina tafsiri nyingine ila ni jaribio la kuwawekea wananchi wa Venezuela serikali inayopendelewa na Washington. Baada ya Marekani kushambulia vikali vituo vya nyuklia vya Iran kwa kutumia mabomu mazito ya kupenya ngome aina ya GBU-57A/B, Machado alimpongeza Donald Trump akidai kuwa “Caracas iko karibu zaidi na Tehran.” Wakati huohuo, alionesha uungaji mkono wa wazi kwa Marekani ilipopeleka meli zake za kivita katika Bahari ya Karibi kwa kisingizio cha kuilinda Israel.
Kimya mbele ya uhalifu
Machado alinyamaza kimya kufuatia mashambulizi ya kifo yaliyofanywa na jeshi la majini la Marekani dhidi ya boti ndogo katika maji ya Karibi, yaliyosababisha vifo vya makumi ya raia kutoka Venezuela na nchi jirani. Ukimya huu, kwa mujibu wa wachambuzi, ni ishara ya kuonesha kwamba kwa vitendo, anashabihiana na siasa dhalimu za Washington dhidi ya utu wa binadamu.
Kutoka mapinduzi hadi usaliti wa mamlaka ya kitaifa
Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, Machado amekuwa mstari wa mbele katika kila mgogoro wa kisiasa nchini Venezuela akiwa upande wa vikosi vya kupinga demokrasia: kutoka kuunga mkono mapinduzi ya mwaka 2002 dhidi ya Hugo Chávez, mgomo wa waajiri wa mwaka 2003, hadi kupinga matokeo ya kura ya maoni ya mwaka 2004. Mwaka 2014, akiwa na Leopoldo López na Antonio Ledezma, alianzisha mpango wa “La Salida” uliolenga kuipindua serikali kwa kuchochea maandamano yenye vurugu. Mwaka 2019, aliunga mkono waziwazi mradi wa Juan Guaidó, na hivyo kuwa mkono wa utekelezaji wa siasa za Washington.
Kuanzia Uribism hadi Uzayuni
Katika miaka ya hivi karibuni, Machado amekuwa akimsifu Álvaro Uribe, rais wa zamani wa Kolombia, ambaye alijulikana kwa utawala wake wa ukandamizaji na mauaji, kiasi cha kuitwa “serikali ya hofu.” Vilevile, kwa majivuno, amezungumzia uhusiano wa chama chake Vente Venezuela na chama cha Likud cha Israel, na katika ujumbe mmoja alisema:
“Leo, wale wote wanaotetea thamani za Magharibi wanasimama bega kwa bega na serikali ya Israel — mshirika wa kweli wa uhuru.”
Ukinzano wa majonzi
Licha ya historia yake wazi ya kuunga mkono vita, ubeberu, na ukandamizaji, jina la Maria Corina Machado limeingizwa katika orodha ya wagombea wa Tuzo ya Amani ya Nobel — tuzo ambayo inapaswa kuwa nembo ya utetezi wa maisha ya binadamu, na si chombo cha kuhalalisha wafuasi wa mauaji ya kimbari na uchokozi wa kivita.
Maoni yako